Friday, June 26, 2009

Michael Jackson Afariki Dunia

Mwanamuziki maarufu wa mtindo wa Pop, Michael Jackson, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 50. Imeelezwa alikimbizwa hospitalini huko Los Angeles, Marekani, baada ya kupata matatizo yanayodhaniwa kuwa ya moyo.

Taarifa za awali zilieleza kuwa mwanamuziki huyo alikuwa hapumui wakati madaktari wa huduma ya kwanza walipofika kumsaidia nyumbani kwake maeneo ya Bel Air yapata saa sita na nusu majira ya huko. Lakini mwishowe maafisa wakathibitisha kifo chake.

Utata mkubwa uligubika hali ya afya ya mwanamuziki huyo aliyewahi kutamba na albamu mbali mbali kama Thriller.

Wavuti ya TMZ ambayo huandika taarifa za watu mashuhuri katika maswala ya burudani ilikuwa ya kwanza kuandika kuwa Michael Jackson mwenye umri wa miaka 50 alikuwa ameaga dunia.

Vile vile, gazeti maarufu la Los Angeles Times liliandika katika wavuti yake kuwa Michael Jackson amefariki. Lakini vyombo vingine vya habari vilikuwa vikisema alikuwa bado yu hai, ingawa alikuwa mahututi.

Madaktari wa huduma ya kwanza walijaribu kuuzindua moyo wa Jackson wakati gari ya wagonjwa ilipokuwa ikimkimbiza katika hospitali ya UCLA, maafisa wameeleza.

Makundi ya watu, wengi wao wakiwa mashabiki wake wamekuwa wakikusanyika nje ya hospitali hiyo, ambako kituo cha wagonjwa wa dharura kimezungushiwa utepe na polisi na baadhi ya barabara kufungwa.

Jackson alikuwa akitarajiwa kuanza matamasha mbali mbali ya kufufua kipaji chake kwenye ukumbi wa O2 jijini London ifikapo tarehe 13 Julai.

Imeelezwa alikuwa na historia ya matatizo ya kiafya na hajawahi kukamilisha ziara ya matamasha kwa kipindi cha miaka 12 iliyopita.

No comments:

Post a Comment